Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amemkosoa Mchekeshaji aliyejizolea umaarufu kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao, Pierre Maarufu kama Mzee wa Liquid mara baada ya kupata mashavu ikiwepo wilayani Kisarawe na Jiji la London nchini Uingereza.
Makonda amesema kuwa watu wa ‘hovyo’ kama Pierre hawapaswi kupewa nafasi kwenye vyombo vya habari.
“Wakina mama kama hawa wanaojituma na kuhangaika kwa ajili ya watoto, wao ndio tuwape kipaumbele, sio hawa walevi walevi, yaani unakuwa na taifa ambalo watu wa hovyo ndio wanakuwa maarufu,”amesema Makonda.
Mkuu wa Wilaya Jokate kupitia ukurasa wake Instagram amemuomba radhi Pierre na kumkaribisha Kisarawe ikiwa ni pamoja na kumpatia fursa ya kutengeneza samani za shule mpya inayotegemewa kujengwa katika Wilaya hiyo.
Aidha, Jokate ameongeza kuwa, “kipekee kabisa nimshukuru Pierre Liquid, wako watu maarufu wengi mno tuliowaalika lakini hawakufika. Ila wewe ulichukua muda wako kuhamamisisha na kufika na zaidi ya hapo ukatoa mchango wa Tsh. Laki moja!!!. Hukuja kuuza sura tu!!. amesema asante sana
Mbali na hilo, Mchezaji wa kulipwa wa klabu ya Tottenham Hotspur F.C. raia wa Kenya, Victor Wanyama amemtaka Pierre aende London yeye na msanii Ommy Dimpoz kwa ajili ya matembezi huku akiahidi kugharamia safari nzima.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla ametaka Pierre aheshimiwe utu wake na kwamba ni mtu huru kwenye nchi yake.
“Jamani maisha ni magumu, yana mitihani mingi na ni mafupi sana. Katika kuleta furaha na shangwe kwenye maisha ndiyo maana ‘wachekeshaji’ wakapata ajira!. Wengine tusome udaktari, uhandisi na tufanye uvumbuzi na utatuzi wa changamoto na wengine watutetemeshe, watuvuruge akili, watupe raha na furaha, watuchekeshe, siku zisogee”, amesema Kigwangalla katika ujumbe wake.
Ameongeza kwamba, “Maisha ndiyo haya haya! Zaidi ya yote, Pierre ni mtu huru kwenye nchi yake. Tunapaswa kuulinda uhuru wa Pierre kama ambavyo Katiba ya nchi yetu inavyoelekeza. Let him be. Tumuache apate riziki yake. Mungu anajua zaidi kwa nini hatukumjua miaka 5 iliyopita na kwa nini sasa anazua mjadala.