Siku chache baada ya kutangaza vita dhidi ya dawa za kulevya na kuanza kuitekeleza kwa kasi, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza vita mpya na makandarasi wasio wawajibikaji.
Makonda ametangaza vita hiyo jana baada ya kuzindua barabara inayotoka Shimo la Udongo kwenda Polisi Ufundi, Kurasini Jijini humo, ikiwa ni siku takribani tisa baada ya kuwa nje ya ofisi yake akidaiwa kwenda nchini Afrika Kusini.
Mkuu huyo wa mkoa ambaye kesho anatimiza mwaka mmoja tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, amesema kuwa hataki kuona barabara zinazoharibika kwa muda mfupi baada ya kujengwa katika mkoa huo.
“Nitakula sahani moja na makandarasi wanaotujengea barabara mbovu. Hao ni halali yangu, sitaki kuona tena Dar es Salaam tuna barabara zinazojaa mashimo, kama ni mashimo yaende kwenye mikoa mingine sio kwenye mkoa huu ninaoutawala,” anakaririwa.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Grand Tech iliyojenga babarabara hiyo yenye urefu wa kilometa moja na kuikabidhi kwa Serikali, Masito Mwasingo amesema kuwa barabara hiyo imegharimu kiasi cha shilingi milioni 350 na kwamba itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwani ilikuwa haipitiki hasa wakati wa misimu ya mvua.