Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania – TASAC, Kaimu Abdi Mkeyenge ametoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu malalamiko dhidi ya Uwakala huo kuvunja mikataba bila kufuata utaratibu.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Machi 10, 2023 jijini Dodoma, amesema taarifa hiyo ilieleza kuwa Mikataba ya mafunzo kazi kwa vijana zaidi ya 400 waliokuwa TASAC, ilivunjwa bila kufuata utaratibu na ikiwa imebaki muda wa mwaka mmoja kuisha kwa mikataba hiyo.
Amesema Vijana hao pia walielezewa kuwa walifanya kazi bila bima ya afya na kwamba TASAC ilitoa rushwa kwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi – CMA, katika mashauri ya kazi yaliyofunguliwa na vijana hao ili haki isitendeke.
“Mnamo mwezi Julai, 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya mabadiliko ya Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania kwa kufuta majukumu ya kipekee ya uwakala wa meli, uhakiki wa mizigo, udhibiti wa nyaraka na kupunguza wigo wa jukumu la kufanya uwakala wa forodha katika bidhaa zilizokuwa zinagombolewa na kuondoshwa na TASAC”, amesema.
Aidha Mkeyenge ameongeza kuwa, “TASAC ilikuwa ikitekeleza majukumu hayo kupitia vijana waliokua wameajiriwa moja kwa moja pamoja na waliokuwa wakifanya mafunzo ya kazi lakini kufuatia mabadiliko, Agosti 11, 2022 TASAC ilivunja mikataba ya mafunzo ya kazi kwa jumla ya vijana 209 waliokuwa wakifanya kazi za uhakiki wa shehena na si zaidi ya 400 kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii.”
Mkeyenge amesema kuwa TASAC haijatoa na haiwezi kutoa rushwa yoyote kwa CMA, ili kuzuia haki isitendeke kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii na kwamba Vijana hao waliandikiwa barua kuwa mikataba yao haitahuishwa tena ifikapo tarehe 30 Agosti, 2022 kutokana na merekebisho ya Sheria ambayo yamesababisha baadhi ya majukumu ya TASAC kufutwa na kuhamia sekta binafsi.
“Kwa mujibu wa masharti ya mikataba, TASAC ilikuwa inawapa mkataba ya miezi mitatu na kuongeza muda kila ilipoonekana inafaa kutokana na utendaji kazi wa mtu,” amesema mkeyenge na kuongeza kuwa mikataba ilikuwa imeainisha utaratibu wa namna ya kuvunja mikataba ya mafunzo kazi na ndio utaratibu uliotumika kuvunja mikataba hiyo.