Baada ya malalamiko ya mwanamuziki Vanessa Mdee, kuhusu kutolipwa pesa zake na kampuni maarufu ya usambazaji wa muziki Afrika Mashariki iitwayo ‘Mziiki’, hatimaye muwakilishi wa kampuni hiyo ametolea ufafanuzi mwenendo mzima wa sakata hilo.
Muwakilishi huyo Kapasta, amefafanua juu ya vipengele mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka wazi njia sahihi ambayo Mdee alipaswa kuifuata, ili kurahisisha suala hilo kumalizika bila usumbufu mkubwa aliopitia katika kudai pesa zake.
“Hili suala Vee yeye amelipeleka mbali, unajua Wahindi mwenendo wa ufuatiliaji wa kazi zake ni kama walikuwa hawauamini, kutokana na watu aliokuwa anawatuma kufuatilia mauzo yake ndio maana walikuwa hawajibu,” amesema.
Amesema, Vanessa amekuwa hapigi simu yeye mwenyewe kuwasiliana na wahusika, na badala yake amekuwa akiwatuma watu, kitendo ambacho wahindi wamiliki wa kampuni hiyo wanakuwa hawawaamini, na wanachodai ni ripoti yake ya kila mwezi, ya malipo.
Aidhwa mwakilishi huyo amesema, “Nimeona ameposti ameonyesha dukuduku lake sio kwa ubaya au amevunja mkataba na hata alichokiandika hakijakaa kwenye ubaya, tatizo ni kuwa anatuma watu tofauti tofauti.”
Amemaliza kwa kusema kuwa, “kwahiyo wao (wamiliki) wanalinda haki yake kwa sababu unaweza ukatoa, kesho yake ukaja ukasema sijatuma mtu so tutamuamini nani?” amesema Kapasta muwakilishi wa kampuni ya ‘Mziiki’ nchini Tanzania.