Taarifa iliyotolewa leo Agosti 27, 2022 na mashirika ya Umoja wa Mataifa imesema, watu 34,000 wameathirika na mafuriko katika majimbo 11 kati ya 23 nchini Chad.

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini New York nchini Marekani, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema tangu Agosti 16, 2022 mafuriko hayo yameshakatili maisha ya watu 22 na kusababisha uharibifu mkubwa wa nyumba, miundombinu, mashamba ya kilimo na kuathiri mifugo.

Ameongeza kuwa, “Pia mafuriko haya yameongeza kiwango cha watu kupata malaria na kuzidisha hofu ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu maana karibu maeneo mengi yaliyoathiriwa hali ni mbaya.”

Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, “Umoja wa Mataifa pamoja na washirika wengine wa kibinadamu wanasaidia juhudi zinazoongozwa na serikali ya Chad kutoa msaada wa kuokoa maisha ikiwemo chakula, huduma za afya, malazi na vifaa vingine vya muhimu.

“Hadi sasa tumeshawafikia watu takriban 30,000 katika majimbo ya East na N’Djamena na tunaongeza juhudi zetu ili kuwafikia watu zaidi na timu ya Umoja wa Mataifa jana ilitoa wito wa msaada wa kifedha kutoka kwa wahisani,” amebainisha Dujarric.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mahitaji ya kibinadamu kabla ya mafuriko hayo nchini Chad yalikuwa yamefadhiliwa kwa asilimia 34 hadi kufikia katikati ya mwezi Agosti, ambapo ni sawa na dola milioni 171 pekee zilizopokelewa kati ya dola milioni 510 zinazohitajika.

Misaada ya kibinadamu yawekewa 'vigingi' Tigray
Malalamiko ya mdee yawaibua Mziiki mafichoni