Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Adam Malima amelitaka Jeshi la Polisi nchini kushirikiana na wadau wa Bima, kuiangalia upya sheria ya Bima ya ulipaji wa fidia pindi ajali zinapotokea ambazo nyingi husababishwa na mwendo kasi, ubovu wa vyombo vya moto, baadhi ya madereva kuendesha wakiwa wamelewa.
Malima ametoa rai hiyo wakati akihitimisha wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani iliyofanyika mkoani Mwanza, na kuzitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na kujaza abiria na mizigo kupita kiasi, kupita gari la mbele bila kuchukua tahadhari na kuegesha magari mabovu yaliyoharibika barabarani kwa muda mrefu.
Amesema, kumekuwa na ucheleweshaji wa malipo ya fidia unaofanywa na baadhi ya makampuni ya Bima kwa wateja wao wanaokata Bima za vifaa vyao hasa vyombo vya moto, na kwamba lengo kuu la maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani ni kutoa elimu ya sheria, kanuni na taratibu za Usalama Barabarani kwa makundi yote ya watumiaji wa barabara.
Kwa mujibu wa Malima takwimu za ajali za barabarani Mkoani Mwanza kwa kipindi cha Januari hadi Desemba, 2022 ajali zilizoripotiwa ni 81, zikisababisha vifo vya watu 71 na majeruhi 96, na ajali za pikipiki ni 30 zilizosababisha vifo vya watu 25 na kujeruhi wengine 26.