Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa ameagiza kufanyika kwa uhakiki wa vyuo vilivyopo Wilayani Mbeya, kufuatia Wazazi, Wanafunzi na Wahitimu wa Chuo cha Mbeya Training kuiomba Serikali iwasaidie kurudishiwa stahiki zao, mara baada ya kubainika kozi ya masomo kutotambulika na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi – NACTIVET.
Baadhi ya wanafunzi chuoni hapo, walitoa maombi hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa na Meneja wa Kanda ya NACTIVET, Joha Fugutilo mara baada ya kuagiza chuo hicho kusimamisha mafunzo kutokana na kukiuka masharti ya uendeshaji.
Katibu Mtendaji wa Nactivet Tanzania, kupitia kwa Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joha Fugutilo mbali na kuagiza chuo hicho kusimamisha utoaji wa mafunzo lakini pia amesema mmiliki asipotoa maelezo ndani ya siku saba chuo hilo kitafutiwa usajili wake.
Wanafunzi wamesema wameiomba Serikali kusaidia kupata Suluhu ya jambo hilo kutokana na wengi wao kupoteza muda wakiwa chuoni hapo na hasara Iliyojitokeza ambapo pia Mkuu wa Wilaya Malisa ameagiza pia vyuo vyote vilivyoko Wilayani kwake kuhakikiwa usajili, ili kUepusha udanganyifu kama huo.
Kwa upande wake mmiliki wa Chuo cha Mbeya Training, Joseph Asajile amekataa kuzungumzia tuhuma hizo zinazomkabili.