Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka msimamo wa uwekezaji wa Bandari kupitia Kampuni ya DP World, akisema malumbano hayawezi kupewa nafasi kwenye mkakati wa kiuchumi.
Rais wa Samia ameyasema hayo wakati wa kuwaapisha Viongozi wateule Ikulu Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mwendelezo wa Serikali kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya watu wanaotumia muda mwingi kurumbana, hali inayochelewesha uwekezaji huo na kutoa mwanya kwa majirani zao kuweka nia ya kupita njia wanayopitia.
Amesema, “wakati sisi tunalumbana bandari apewe nani iende isiende, ikae, ivue isivue, wenzetu kwa kuona malumbano yetu wame-jump wamekwenda kulekule, lile lile jumba lilowekwa bendera ya Tanzania limewekwa bendera ya jirani, sasa Tanzania tumeuza wale jirani wamekimbilia kule kufanya nini?.”
Mara baada ya Serikali kutangaza mpango wa kuwekeza kwenye bandari ya Dar es Salaam, baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wamekuwa wakipinga, hali iliyowaibua baadhi ya Viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa ujenzi na uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, huku Rais Samia akitoa ufafanuzi huo hii leo Julai 14, 2023.