Mama Mzazi wa Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’, amepaza sauti na kulitaka Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ kutenda haki dhidi ya mtoto wake.
Mama Feisal amefanya hivyo, zikisalia saa chache kabla ya Marejeo ya Kesi ya kimkataba kati ya Kiungo huyo na Klabu ya Young Africans, mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.
Mama huyo amedai kuwa Mwanawe amekuwa na wakati mgumu ndani ya Klabu ya Young Africans, na maamuzi ya kuondoka kwake klabuni hapo yalikuwa sahihi, na yamepata baraka zote za familia.
“…Tunaomba TFF watende haki,huyu mtoto apate haki yake,TFF na wao ni binadamu na ni wazazi hivyo hakuna Mzazi ambaye anapenda mwanawe apate matatizo.”
“Mimi sikusema kwamba Feisal arudi Yanga kumalizia mkataba,sikusema na sitosema kwakuwa mimi ndio nilioona shida aliyopata mwanangu na aliteseka sana Yanga mpaka kuamua uamuzi huo mzito…”
“Fei kateseka sana Yanga, kaishi Mazingira magumu,Fei sio mwendawazimu,kaamua kudai haki yake imekua kosa?”
“Msimamo wa Familia kwa ujumla tunataka Fei aondoke Yanga aende mbele akatafute changamoto kwingine kwajili ya hatma yake ya baadae” amesema mama Feisal
Marejeo ya Kesi baina ya Feisal Salum na klabu ya Young Africans yanafanyika leo Alhamis 2/03/2023 badala ya tarehe 27/02/2023 Kama ambavyo zilielezwa pande zote mbili, Sababu ikiwa ni kutotimia kwa akidi ya Wajumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.
Awali kamati hiyo ilikuwa ikutane tarehe 15/02/2023 Kabla ya Mabadiliko hayo ya tarehe kufanyika mara mbili.