Mama Salma Kikwete, mke wa rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete ametoa nasaha zake kwa Ali Kiba na Abdu Kiba kwenye sherehe ya ndoa ya ndugu hao waliooa siku moja, iliyofanyika usiku huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mbele ya maharusi hao, moja kati ya mambo aliyowatahadharisha ni hatari ya simu za mkononi katika maisha ya ndoa. Aliwataka maharusi hao kuhakikisha hawaigeuzi simu kuwa siri inayofichwa kwa nguvu zote.
Aliwataka kuiga maisha yake na Dkt. Kikwete ambayo kwa ujumla wake simu yake ni simu ya mumewe na simu ya mumewe vilevile ni kama simu yake.
“Mkiangalia simu mtaachana kabla ya siku nyingi, aminianeni. Mkiaminiana basi maisha yatakuwa mazuri, lakini kila wakati ukifika nyumbani unaanza kupekuwa nani ametuma nini…. kwa mfano wakati mwingine simu ikilia unakosa amani ya roho. Kwanini kuwa mtumwa wa aina hiyo?” Alisema.
“Mimi simu ya mume wangu naipokea, na mume wangu simu yangu anaipokea. Na sio kama nimeanza leo, tangu siku ya kwanza hizi simu zilipoingia… mimi sifichi simu. Kwahiyo kuweni huru na simu zenu, msifichefiche na msiweke kwenye maziwa mtapata maradhi kwa sababu tu ya kuficha,” aliongeza Mama Salma.
Katika hatua nyingine, aliwahusia wanandoa hao wapya kuhakikisha wanajiweka mbali na maisha yanayoweza kuwaweka katika hatari ya kupata maradhi kama ukimwi.
Mama Salma ambaye pia alifika na familia yake aliyoitambulisha, alifikisha pia salamu za Dkt. Kikwete ambaye kutokana na majukumu mengine na kuwa njia ya nchi alishindwa kuhudhuria harusi hiyo.
Harusi hiyo ya kwanza ya watu maarufu nchini kufunga ndoa kwa siku moja ndugu wa damu moja imehudhuriwa na watu wengi maarufu na viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu pamoja na Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde.
Pia, Gavana wa Mombasa ambaye ni rafiki mkubwa wa Ali Kiba alihudhuria akiongozwa na ugeni wa watu kadhaa kutoka nchini Kenya.
Vanessa Mdee, Christian Bella, Mwana Fa, Ommy Dimpoz, Emmanuel Okwi, Nadir Canavaro, Himid Mau Mkami, Vanessa Mdee, Mimi Mars, Milard Ayo, Gerald Hando ni kati ya watu maarufu waliohudhuria.