Benki ya CBA ikishirikiana na kampuni ya Vodacom imefanya droo yake ya tano ya kufikisha miaka mitano ya huduma ya M-Pawa yenye lengo la kuongeza ushirikishwaji wa kifedha kwa wateja wake.
Meneja Masoko wa CBA, Solomon Kawiche amesema kuwa katika maadhimisho ambayo yamefanyika kwenye makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es salaam, yaliambatana na sherehe mbalimbali ikiwemo droo za kila wiki zilizohusu kuwekeza na kukopa kupitia M-Pawa ambapo washindi 340 walipatikana wakiwa na mara mbili ya akiba zao kuanzia kiwango cha shilingi 1000-200,000 na simu janja pamoja na muda wa maongezi.
Kawiche amesema kuwa M-Pawa ilianza na wateja wanne na hadi kufikia sasa imefikisha wateja milioni 8.5 na kufanikiwa kurahisisha maisha ya wananchi wengi ambao wapo mbali na huduma za kibenki kwa kuwapatia huduma hizo kwa unafuu ikiwemo kuweza kukopa kiasi kidogo cha fedha cha shilingi 1000 ambacho ni aghalabu kukipata kupitia huduma za kibenki kwenye benki zingine.
Amesema kuwa M-Pawa imefanikiwa kutoa huduma ya kuhifadhi akiba kwa kiwango cha chini ambacho ni Tsh. 1, na kuifanya CBA kuwa benki pekee ya ndani ya Tanzania ambayo inatoa huduma hiyo na kurahisisha huduma za kibenki bila ya kuwa na utaratibu mrefu katika kukamilisha miamala.
Pia ameongeza kuwa uwepo wa usalama wa fedha za wateja wao pamoja na kutokuwepo kwa makato kwenye fedha za watumiaji wa huduma hizo kupitia M-Pawa kumewaondolea wateja wao gharama za kutembelea kwenye matawi yao na kupitia huduma hiyo wateja hao wanapata faida kupitia akiba zao.
Meneja huyo wa masoko wa benki hiyo ameongeza kuwa huduma hiyo imeinua hali ya maisha ya mamilioni ya Watanzania hususani wafanyabiashara wadogo na bila kusahau kuwa imekua ikitoa uhakika wa kifedha wakati wa dharula ambapo mteja anaweza kukopa muda na wakati wowote.
“Kama benki tuna malengo ya kuwekeza zaidi kwenye huduma hii kuhakikisha kuwa inaendana na maendeleo ya sasa ya kisayansi na teknolojia na kuwezesha huduma hii kwenye ‘application’.