Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amefanya mabadiliko madogo kwa baadhi ya viongozi ndani ya Jeshi la Polisi ambapo amemhamishia Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Lazaro Mambosasa kutoka kuwa kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na kwenda kuwa Mkuu wa Operesheni Dodoma.
Katika barua iliyosainiwa kwa niaba yake na Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu, imeeleza kuwa IGP amemhamisha pia aliyekuwa Mkuu wa Operesheni Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Camilius Wambura kuwa Kamanda wa Polisi Dar es Salaam.
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Daniel Shillah amebadilishiwa kituo cha kazi kutoka kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara na kuwa Mkuu wa Upelelezo (ZCO) Kanda Maalum Dar es Salaam huku nafasi anayoaacha Mara ikichukuliwa na Kamishna Msaidii Longinus Tibishibwamu.
Pia, IGP amembadilishia majukumu Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Optatus Maganga kutoka OCD wa Wilaya ya Makete na kuwa Kamanda wa Polisi Njombe.