Mamilioni ya wananchi wa Venezuela wameripotiwa kujiunga na maandamano ya kupinga hatua ya serikali ya Rais Nicolás Maduro kuahirisha uchaguzi.
Mapambano kati ya waandamanaji na jeshi la polisi yamesababisha vifo vya watu watatu huku zaidi ya watu 300 wakishikiliwa na jeshi hilo. Kwa mujibu wa BBC mabomu ya machozi ya kuwatuliza waandamanaji yamefyatuliwa katika baadhi ya majiji.
Viongozi wa upinzani waliohamasisha maandamano hayo wameeleza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Wananchi wamejiunga na maandamano katika mitaa ya majiji na miji mbalimbali.
Hata hivyo, Serikali ya Rais Maduro imeeleza kuwa maandamano hayo yako katika kiwango cha chini na kwamba wananchi wanaendelea na shughuli zao za kawaida, maduka yakiwa yamefunguliwa na wafanyakazi wa umma wakienda ofisini kama kawaida.
Rais Maduro ametangaza kuwa atahakikisha kuwa waanzilishi wa maandamano hayo watakamatwa wote na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Maandamano yalianza tangu Aprili mwaka huu ambapo ripoti inaeleza kuwa tangu wakati huo takribani watu 100 wamepoteza maisha nchini Venezuela.