Umoja wa vyama vya upinzani wa National Super Alliance (Nasa) nchini Kenya umepata pigo baada ya kesi yao ya kupinga zabuni ya karatasi za kupigia kura kupewa kampuni moja ya Dubai kutupiliwa mbali na Mahakama Kuu.

NASA walifungua kesi katika mahakama kuu dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) ikipinga uamuzi wake wa kuipa zabuni ya kuandaa karatasi hizo kampuni ya Al Ghurair iliyoko nchini Dubai kwa madai kuwa haikufuata taratibu za manunuzi ya umma na kwamba ililenga kuwafaidisha umoja wa chama tawala wa Jubilee.

Jopo la majaji watano wa Mahakama kuu liliamuru zabuni hiyo kuendelea kwa njia ya manunuzi ya moja kwa moja kwa kuipa kampuni ya Al Ghurair bila kufuata utaratibu wa kutangaza zabuni na kuingia katika ushindani.

“Tumebaini kuwa njia ya kufanya manunuzi moja kwa moja iliyotumiwa na IEBC haikuwa na nia ya kuepuka ushindani bali ilitokana na ufinyu wa muda kuelekea tarehe ya uchaguzi,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo.

Mahakama Kuu iliongeza kuwa zabuni hiyo ya karatasi za kupigia kura haiwezi kugawanyika kwani ni ya aina moja, hivyo njia ya ushindani haikuwa na ulazima na kwamba sababu za IEBC zilikuwa na mashiko.

Kesi hiyo ilifunguliwa na NASA ambao waliiomba Mahakama Kuu kufuta mpango wa kufanya manunuzi ya karatasi hizo moja kwa moja kwa Al Ghurair.

Nasa wakuwa wakilalamika majukwaani kuwa wana mashaka na uhusiano kati ya wamiliki wa kampuni hiyo na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa serikali ambao wako katika kambi ya Jubilee.

Mamilioni wajiunga na maandamano Venezuela, yasababisha vifo
Video: Polisi wamvuruga Lissu, Magufuli azuia Warundi kupewa uraia nchini