Mamlaka ya Mawasiliano na Vyombo vya Habari nchini Sudan Kusini imeifungia redio Miraya ambayo inamilikiwa na Umoja wa Mataifa kwa madai ya kutozingatia sheria ya vyombo vya habari ya nchi hiyo.
Msemaji wa Mamlaka hiyo, Alijah Alier Kuai amesema kuwa kituo hicho cha redio kimekuwa kikaidi dhidi ya sheria na taratibu za vyombo vya habari na kwamba kimefanya hivyo kwa muda mrefu.
Kuai ameongeza kuwa kituo hicho kimekataa kujibu barua za madai mengi zinazotolewa na Mamlaka hiyo ikikitaka kujieleza.
Aidha, amesema ukaidi wa kituo hicho dhidi ya sheria na kanuni umewekwa nyuma ya mgogo wa madai kuwa ni kandamizi.
Msemaji wa misheni za Umoja wa Mataifa nchini humo, Fransisco Molde ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa wanafanya mazungumzo na Serikali lakini watakuwa wakiendelea kurusha matangazo wakati mazungumzo yakiendelea.
Vyombo vya habari nchini Sudan Kusini vimekumbwa na kibano na wakati mwingine kuwa hatarini kufungiwa daima tangu kutungwa kwa sheria na kanuni za vyombo vya habari mwaka 2016.
Mwaka jana, Mamlaka hiyo iliwafungia waandishi wa habari 20 wa kimataifa kutoripoti chochote kuhusu nchi hiyo wawapo ndani. Vyombo kadhaa vya habari nchini humo pia vilifungiwa.