Kupitia ukurasa wake mtandao wa kijamii wa Instagram, Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), wametangaza nauli mpya za mabasi ya mwendo wa haraka zitakazoanza kutumika rasmi kuanzia Jumatatu, Januari 16, 2023 huku nauli kwa Wanafunzi zikibaki kama zilivyo.
Katika ukurasa huo, DART imeandika kuwa, “Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), unapenda kuwaarifu watumiaji wa mabasi yaendayo haraka kuwa kuanzia Jumatatu, Januari 16, 2023 nauli mpya zilizoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) zitaanza kutumika.”
Taarifa hiyo imeonyesha kuwa nauli katika njia kuu ya Kimara-Kivukoni, Kimara-Gerezani na Kimara-Morocco itakuwa Shilingi 750 wakati Kimara-Mbezi nauli itakuwa Shilingi 500 na njia ya Kimara – Kibaha na Kimara-Mlongazila itakuwa Shilingi 700, huku Gerezani –Muhimbili ikiwa Shilingi 750.
Aidha, nauli mpya za taksi mtandaoni, LATRA imeelekeza teksi zinazobeba abiria wanne nauli kuwa Shilingi 3,000 hadi 4,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama safari itaongezeka toka hapo nauli itakuwa Shilingi 800 hadi 1,000 kwa kilomita moja na safari inapokutana na vikwazo kama foleni nauli ya ziada itaongezeka kwa Shilingi 80 hadi 100 kwa dakika.
Kwa upande wa magari yanayobeba abiria sita nauli elekezi ni Shilingi 4,000 hadi 5,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kutakuwa na safari ya ziada nauli itaongezeka kwa Shilingi 1,000 hadi 1,200 kwa kilomita moja na kama kuna foleni nauli itaongezeka Shilingi 80 hadi 150 kwa dakika.
Kuhusu Pikipiki ya kubeba abiria wawili nauli elekezi ni Shilingi 1,000 hadi 1,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja na ikiongezeka kutoka hapo nauli itaongezeka kwa Shilingi 300 hadi 400 kwa kilomita moja na iwapo kutakuwa na vikwazo au foleni nauli itaongezeka Shilingi 50 hadi 70 kwa dakika.