Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka England Man City wameshindwa kutamba katika mchezo wao dhidi ya Newcastle United baada ya kutoka sare ya mabaoa mawili kwa mawili, mchezo uliopigwa Uwanja wa St. James’ Park leo Jumamosi.
Mchezo huo ulikuwa na umuhimu kwa meneja wa Man City Pep Guardiola kupata pointi tatu, kutokana na hitaji lake la kutaka kukaa nyuma ya vinara Liverpool wanaoongoza msimamo wa ligi ya England kwa sasa.
Kwa sasa Man City wamesogea katika nafasi ya pili kwa kufikisha alama 29, lakini wapo mbele kwa mchezo mmoja dhidi ya Leicester City wenye alama 29.
Katika mchezo wa leo Man City ndio walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia Raheem Sterling dakika 22 lakini Newcastle walichomoa dakika 25 kupitia Jetro Willems.
Baada ya bao hilo mchezo ulikuwa mgumu huku kila kikosi kikitengeneza nafasi lakini kulikuwa na ugumu wa kuingia katika safu ya ulinzi na wote kutumia mashuti kwenda golini.
Dakika 82, Kevin De Bruyne aliifungia Man City bao la pili kwa shuti kali lililokwenda moja kwa moja wavuni na kuwafanya kutangulia mbele mabao mawili kwa moja.
Bao hilo ni kama liliwaongezea morali wachezaji wa Newcastle baada ya kutoonekana kukata tamaa na kuendelea kutengeneza mipango ya kushambulia.
Dakika 88 Jonjo Shelvey aliisawazishia Newcastle na matokeo ya mabao 2-2 hali iliyomfanya Guardiola kwenda vyumbani haraka haraka.