Bodi ya Ligi Kuu ya England ‘Premier League’ imeishtaki Klabu ya Manchester City kwa ukiukaji zaidi ya 100 wa sheria zake za kifedha kufuatia uchunguzi wa miaka minne.
‘Premier League’ imeipeleka klabu hiyo mbele ya tume huru kwa madai ya kukiuka kanuni kati ya mwaka 2009 na 2018.
Bodi hiyo pia imeishutumu Manchester City kwa kutoshirikiana tangu uchunguzi uanze mnamo Desemba 2018.
Msimu uliopita City ilishinda taji lao la sita la Ligi Kuu tangu ilipoanza kuwa chini ya mmiliki Abu Dhabi United Group mwaka 2008.
Kufautia tuhuma hizo, Klabu ya Manchester City huenda ikakutana na adhabu ya kutozwa faini, kukatwa alama na kuondolewa kwenye orodha ya Klabu za Ligi Kuu ya England.
Katika taarifa yake, ‘Premier League’ imeeleza kuwa Manchester City ilikiuka sheria zinazowataka kutoa taarifa sahihi za kifedha zinazotoa mtazamo wa kweli na wa haki wa hali ya kifedha ndani ya klabu hiyo.
Maelezo haya yalihusisha mapato ya klabu hiyo, ambayo yanajumuisha mapato ya udhamini na gharama za uendeshaji.
Ukiukaji zaidi unaodaiwa kuhusiana na sheria zinazohitaji maelezo kamili ya malipo ya meneja kutoka misimu ya 2009-10 hadi 2012-13, wakati Roberto Mancini alikuwa madarakani na malipo ya wachezaji kati ya 2010-11 na 2015-16.
Premier League imeeleza Manchester City ilikiuka kanuni zinazohusiana na kanuni za Shirikisho la Soka Barani Ulaya UEFA, ikiwa ni pamoja na Financial Fair Play (FFP), kuanzia 2013-14 hadi 2017-18, pamoja na kanuni za Ligi Kuu kuhusu faida na uendelevu kuanzia 2015-16 hadi 2017-18.
Mnamo 2020, Shirikisho la Soka Barani Ulaya UEFA liliamua kwamba City ilifanya “ukiukaji mkubwa” wa kanuni za FFP kati ya 2012 na 2016.
Uefa ilianza uchunguzi wake kuhusu City baada ya gazeti la Ujerumani Der Spiegel kuchapisha nyaraka zilizovuja mnamo Novemba 2018 zinazodai kuwa klabu hiyo ilikuwa imeongeza thamani ya mkataba wa udhamini.
Shughuli za tume hiyo inayoongozwa na Murray Rosen KC zitakuwa za siri na kusikilizwa kwa faragha.
Uchunguzi wa Ligi Kuu ulipoanza, City ilisema madai hayo ni “uongo kabisa” na kwamba madai katika Der Spiegel yalitokana na “udukuzi usio halali na uchapishaji wa barua pepe za City”.
Klabu hiyo bado haijatoa maoni yoyote juu ya mashtaka ya Bodi ya Ligi Kuu ‘Premier League’.