Kikosi cha Man Utd kimesonga mbele katika michuano ya Europa League baada ya kuichapa FC Rostov bao moja kwa sifuri, katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora uliochezwa Old Trafford usiku wa kuamkia leo.
Kiungo mshambuliaji kutoka nchini Hisapnia Juan Mata alifunga bao hilo pekee la Man Utd katika mchezo huo, ambao ulionekana kuwa na upinzani mkubwa kutokana na kila upande ulihitaji ushindi.
Ushindi wa bao moja kwa sifuri unaivusha Man Utd hadi kwenye hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao mawili kwa moja.
Katika mchezo wa mkondo wa kwanza ambao ulichezwa nchini Urusi juma lililopita, timu hizo zilitoshana nguvu kwa kufungana bao moja kwa moja.
Katika hatua nyingine kiungo wa Man Utd Paul Pogba, hakumaliza dakika 90 za mchezo wa jana baada ya kupata majeraha ya misuli ya paja na nafasi yake ilichukuliwa kiungo kutoka nchini Ubelgiji Marouane Fellaini.
Matokeo ya mchezo mwingine ambao ulishuhudia mchezaji wa Tanzania Mbwana Samatta akipambana sambamba na kikosi cha klabu yake ya Genk dhidi ya wapinzani wao Gent, ulimalizika kwa sare ya bao moja kwa moja.
Sare hiyo inaiuvusha klabu ya Mbwana Samatta kwa jumla ya mabao sita kwa matatu.
Matokeo ya michezo mingine ya Europa league.
Besiktas 4 – 1 Olympiacos (5-2)
FC Krasnodar 0 – 2 Celta Vigo (1-4)
Ajax 2 – 0 FC Koebenhavn (3-2)
Anderlecht 1 – 0 APOEL Nicosia (2-0)
Borussia Moenchengladbach 2 – 2 Schalke 04 (3-3), Schalke imepita kwa faida ya bao la ugenini
Roma 2 – 1 Lyon (5-4)
Muhimu: kwenye mabano ni jumla ya mabao baada ya kuchezwa michezo ya mikondo miwili.
Ratiba ya hatua ya robo fainali itapangwa baadae hii leo katika makao makuu ya shirikisho la soka barani Ulaya UEFA mjini Nyon nchini Uswiz.