Uongozi wa klabu ya Manchester United umewataka wachezaji wake walioko nje ya England, kurejea nchini humo juma hili tayari kwa kuanza mazoezi kufuatia mipango ya kurejea kwa ligi mwezi Juni mwaka huu.
Baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ambao waliondoka England kwa ruhusa maalum ni pamoja na Bruno Fernandes, Fred, Victor Lindelof na Sergio Romero.
Baadhi ya vilabu nchini humo tayari vimeanza mazoezi na vimependekeza ligi kuanza mwezi Juni katika viwanja huru, mapendekezo ambayo bado yanasubiri uamuzi wa serikali unaotarajiwa kutolewa Mei 10 mwaka huu.
Tayari wachezaji wa klabu za Arsenal na West Ham wameshaanza mazoezi ya pamoja, na klabu hizo zimekua klabu pekee zilizoanza utaratibu huo wa kujiandaa na michezo iliyosalia. Hata hivyo kuna uwezekano mdogo wa ligi kuu Uingereza kuhairishwa kama ligi nyengine haswa kutokana na hasara inayotajwa kufikia zaidi ya paundi milioni 800 kama ligi hiyo ikihairishwa.
Hadi ligi kuu ya England inaahirishwa, Liverpool walikua kileleni kwa kufikisha alama 82, wakifuatiwa na Manchester City [Alama 57], Leicester City inashika nafasi ya tatu [Alama 53] huku Chelsea ikiwa nafasi ya nne [Alama 48].