Vita kali ya maneno imeibuka katika mitandao ya kijamii baina ya wasemaji wa klabu kongwe za Tanzania Simba SC na Young Africans, kufuatia maamuzi ya mkwaju wa Penati yaliyochukuliwa na Mwamuzi Ahmada Simba.

Jana Alhamis (Februari 03) Simba SC iliikaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam na kupata ushindi wa 1-0 kwa pigo la Penati.

Dakika 90 za mchezo huo zilipomalizika Msemaji wa Young Africans Haji Sunday Manara aliibuka kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuonesha hakubaliani na pigo la Penati ya Simba SC lililoamuriwa na Mwamuzi Ahmada Simba.

Manara aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram huku ujumbe wake ukisindikizwa na picha ya Mwamuzi wa mchezo wa Simba SC dhidi ya Tanzania Prisons ( Ahmada Simba).

Manara aliandika: “Vp GSM anahusika au?”

“Caption haina uhusiano na Picha ya juu,,,,huwa napenda tu kuwapost Waungwana Marefarii wetu”

Hata hivyo andiko hilo la Haji Manara lilijibiwa na Meneja wa Habari na Mawasilino Simba SC Ahmed Ally kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagarm, huku akiweka video ya mchezo wa Young Africans dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa mapema msimu huu 2021/22.

Ahmed Ally aliandika: “Wanaojifanya watetezi wa wanyonge, Walinyonga mtu hadharani bila aibu…”
“Masikini Ruvu Shooting walipitia uchungu mkali sana”

“Tukianza kukagua mechi moja baada ya nyingine mtabaki na point 8 tuu nyie”

Manara akarudi tena kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuweka Video ya mchezo wa Young Africans dhidi ya Ruvu Shooting uliochezwa msimu wa 2016/17 na kuandika: “Sikumbuki sawa sawa huyu Mwamuzi bora kabisa, niliwahi kumuona akichezesha mechi flani hivi, katika Siku za karibuni, ila sikumbuki game gani?”
“Nikumbushe”

Ahmed Ally akarudi tena, lakini hakuonesha kama anajibu ujumbe wa Msemaji mwenzake na badala yake akageukia kwa mashabiki wa Simba SC kwa kuwapa shukuruni.

Ujumbe wa Ahmed Ally kwa mashabiki: “Asanteeni sana mashabiki wa @simbasctanzania kwa kuendelea kuiunga mkono timu yetu hamjawahi kuchoka wala kukata tamaaa.”

“Jumapili hii tuna jambo letu jingine palepale kwa Mkapa dhidi ya Mbeya Kwanza.”

“Insha Allah Tatu nyingine hizi kutoka Mbeya”

Ijumaa Kareem

Chozi la CEO wa Facebook Mack Zuckerbeg
Rais Samia atengua uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri 4