Baada ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, Mwenyekiti wa klabu hiyo Mlataza Mangungu ametamba kwa maneno ambayo yanatia hasira kwa timu pinzani.
Mangungu ambaye aliingia madarakani mwanzoni mwa mwaka huu, baada ya kuchaguliwa na wanachama wa Simba SC, huku akimshinda Juma Nkamia, amesema tangu alipoingia madarakani alikua anaamini hakuna klabu itakayowatisha katika harakati za kutetea taji lao.
Amesema sababu kubwa ya kujiamini hivyo, ni kuwa na kikosi imara pamoja na benchi la ufundi linalofahamu mbinu kadhaa za kupambana na timu pinzani, hivyo alikuwa anasubiri muda wa kuiona Simba ikikaa kileleni, hatua ambayo kwake anaamini ndio ufunguo wa kutwaa taji kwa mara ya nne mfululizo.
“Tulikuwa bize na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ndio maana walikuwa wanaongoza katika msimamo lakini bila ya hivyo wangeishatupisha muda mrefu sana,”
“Simba hii haigusiki, hakuna wa kutupokonya ubingwa sijamuona hata mmoja, Simba inamalengo yake ambayo imejipangia toka ligi haijaanza, na huu ni msimu wa nne tunalitwaa taji mfululizo na tutaendelea hivyo hivyo,”amesisitiza Mangungu.
Amesema kazi yao Uongozi ni kuhakikisha wanaweka mipango madhubuti ambayo itazidi kuwafanya wachezaji wao kuwa bora muda wote na kuzidisha ushindani zaidi na zaidi.
Simba SC inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 58, na leo saa moja usiku itacheza mchezo mwingine wa ligi hiyo dhidi ya Dodoma Jiji FC, Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.