Siku mbili baada ya Katibu wa Kamati ya Muafaka ya Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali kusema kuwa Yanga haiwezi kukodishwa kama masufuria ya kwenda shughulini, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji amezungumza kuhusu mkutano mkuu wa Yanga na kugusia kuhusu ushiriki wa Mzee Akilimali kama atashiriki au hatashiriki.

Manji amesema kuwa kuna taarifa ameiona sehemu ikielezea kuwa Mzee Akilimali hajalipa ada ya uanachama wa Yanga na hilo kama lina ukweli basi kwa mujibu wa katiba ya Yanga hataruhusiwa kushiriki mkutano huo ambao utafanyika Jumapili.

“Nimeona habari sehemu imesema kuwa hajalipa ada ya uanachama kwa miezi sita, sina hakika ila kama ni kweli hataruhusiwa kushiriki kwenye mkutano, na hilo sijalipanga mimi ni katiba ya Yanga ndiyo inasema hivyo, mimi sina mamlaka ya kupindisha katiba,” amesema Manji.

Aidha Manji amezungumza kuhusu mkutano mkuu na kuwataka wanachama wa Yanga kujitokeza kwa wingi ili waweze kufanya maamuzi ya pamoja ambayo yatakuwa na faida kwa klabu na kwa ambao bado hawajasoma taarifa ya makubaliano ya Yanga na kampuni ya Yanga Yetu basi watapatiwa taarifa hizo wazisome kabla ya mkutano.

“Kama mwanachama hajalipa kadi kwa kipindi cha miezi sita afike kwa viongozi wa matawi kuomba tena nafasi ili ikiwezekana na yeye ahudhurie mkutano, wanachama waje tujue ni maamuzi gani tutafanya, ulinzi upo wa kutosha na ambao bado hawajasoma taarifa wanaweza kufika ofisi za klabu saa 7:30 asubuhi tutakuwa tumeshafungua ofisi,” alisema Manji.

Kampuni ya TANMAT yatozwa faini ya sh. mil.50 kwa uchafuzi wa mazingira
Waziri Mkuu arejea Dar akitokea Arusha.