Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imethibitisha kuwa inamshikilia mfanyabiashara Yusuph Manji kwa mahojiano.

Manji, ambaye aliondoka nchini mwaka 2018 baada ya Serikali kuondoa nia ya kuendelea na kesi iliyokuwa ikimkabili, amerejea juzi jioni na baada ya kukamilisha taratibu za uhamiaji akachukuliwa na maofisa wa TAKUKURU.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni amesema wanamshikilia Manji kutokana na tuhuma tatu zinazomkabili.

Hamduni amesema kabla ya Manji kutoroka nchini kuna uchunguzi ulifanywa kuhusu kampuni zake za Intertrade Commercial Ltd Services na Golden Globe International Services Limited.

Kampuni zake za Intertrade Commercial LTD Service na Golden Globe International Service Limited zinatuhumiwa kwa kutolipa kodi ya VAT kati ya mwaka 2011 na 2015 wakati zikifanya biashara na Shirika la Umeme nchini Tanzania Tanesco Kupitia kampuni yake ya Golden Globe.

Kamishana Hamduni anasema kulifanyika udanganyifu wakati wa manunuzi ya kampuni ya Tigo.

Tuhuma nyingine inayomkabili ni kupitia kampuni yake ya Quality Group kuhusu mapato ya klabu ya Yanga ambayo alikuwa akiidhamini na kuiongoza kama mwenyekiti wakati huo.

Manji alitorokea nje ya nchi mwaka wa 2018 baada ya Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es salaam kumuachia huru pamoja na wenzie watatu mwezi Septemba 2017 walipokuwa wakituhumiwa kwa makosa saba ya uhujumu uchumi.

Alituhumiwa pia kuhujumu usalama wa taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotengeza sare za jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 za Kitanzania.

Manji amerejea nchini Tanzania siku chache baada ya Rais Samia Suluhu kuhimiza wafanyabiashara waliotoroka nchi kurejea na kuendelea na uwekezaji wao.

Mwanafunzi wa chuo amnyonga mpenzi wake
TANePS yasaidia kuongeza ukidhi wa sheria, kuokoa fedha za umma