Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Mfaume Mfaume ‘Mapafu ya Mbwa’ anatarajia kupanda ulingoni dhidi ya Nkululeko Mhlongo raia wa Afrika Kusini katika pambano linalotarajia kupigwa Juni 30, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar.
Mfaume anarejea ulingoni ikiwa imepita miezi sita tangu alipopanda ulingoni Desemba mwaka jana katika pambano lililovunjika dhidi ya Idd Pialali kwa madai ya kupigana vichwa ambapo atarejea ulingoni kwenye pambano hilo lililopewa jina la Hata Usipolala Patakucha.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Paf Promotion Entertainment Company Ltd, Fadhili Maogola inayomsimamia bondia huyo amesema Mfaume atarejea ulingoni Juni 30, mwaka huu katika pambano walilomuandalia dhidi ya Nkululeko Mhlongo kutoka Afrika Kusini yakiambatana na mapambano mengine ya utangulizi.
“Sisi Paf Promotion Entertainment Company Ltd tumeanza kazi ambayo tumehaidi kwa muda mrefu wa kuandaa pambano kali la kimataifa kati ya Mfaume Mfaume au Mapafu ya Mbwa dhidi ya Nkululeko Mhlongo kutoka Afrika Kusini.”
“Tumeanza maandalizi na tayari bondia ameshaingia kambini kufanya maandalizi pamoja na mabondia wengine ambao watacheza mapambano ya utangulizi lakini kwa upande wetu kama waandaji tunaendelea na maandalizi pamoja na kutafuta wadhamini ambao bado milango ya kudhamini ipo wazi tunawakarihisha kwa wingi kwa sababu hii kwetu ni mara ya kwanza kufanya tukio la aina hii,” amesema Maogola