Kazi ya kupambana na matumizi ya Dawa za kulevya inahitaji nguvu ya pamoja kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. – DCEA, kushirikiana na Vyombo vya Habari kuielimisha jamii kiufasaha, ili kupunguza madhara kwa jamii na kuimarisha nguvu kazi ya Taifa.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam hii leo Novemba 14, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Nchini – TBC, Dkt. Ayub Rioba katika Semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari inayotolewa na DCEA, ambapo amesema madhara yatokanayo na matumizi ya Dawa hizo ni makubwa na kwamba ni ushirikiano pekee utasaidia kupunguza tatizo hilo.
Amesema, ” kwanza kuna maswali ya kuuliza, kwani mtu akivuta Bangi kuna tatizo gani, hela yake, raha anapata yeye, kuathirika ataathirika yeye ninyi DCEA inawahusu nini, mnamkataza ili iweje? je Waandishi wa Habari huwa mnayauliza maswali kama haya? jitahidini myajue ili mkipata majibu muielimishe jamii kiufasaha maana tatizo ni kubwa.”
Dkt. Rioba ameongeza kuwa licha ya mapambano kuendelea lakini hali ya utumiaji wa Dawa za kulevya bado inaendelea hivyo ni muhimu kuweka mkazo katika uelimishaji na kushirikisha jamii kwa kufuatilia yanayotokea na kuyaeleza kwa kushirikiana na Mamlaka husika.
“Maaskofu wanapiga kelele, Ma-Sheikh wanakemea jamii inalisemea hili lakini hali bado si shwari, ni kweli haiwezekani kwa siku moja tatizo hili kukoma lakini kwa ushirikiano na Vyombo vya Habari kusimama katika uelimishaji inawezekana kabisa kuibadilisha hii hali na kupunguza madhara,” amebainisha Dkt. Rioba.
Hata hivyo, amesema zipo athari zinazojitokeza kwa jamii na kwamba watumiaji wengi huarhirika kiafya na hata wauzaji kutumia pesa walizonazo kupindisha haki, hivyo ni muhimu kuendelea kulipambania jambo hilo bila kuchoka ili kuleta mabadiliko, na Vyombo vya Habari vina nafasi kubwa ya kufanikisha jambo hilo.