Taasisi ya Elimu Tanzania – TET imewasilisha mapendekezo ya muundo wa elimu na mabadiliko yaliyopo kwenye Rasimu ya mitaala mipya ya elimu kwa bodi na menejimenti ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi – VETA, katika chuo cha Utalii cha VETA jijini Arusha.
Pendekezo hilo limewasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania – TET, Dkt. Aneth Komba mbele ya Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Sifuni Mchome, wajumbe wa bodi na menejimenti ya VETA, ambapo ameeleza kuwa mitaala mipya itasaidia kumuandaa Mwanafunzi kujitegemea.
Amesema, “maboresho haya ya Mitaala mipya ya elimu yamefanyika kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha elimu itakayomuwezesha muhitimu kuweza kujiajiri na kuajiriwa baada ya kumaliza masomo yake.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Prof. Mchome ameeleza kuwa wasilisho la Mitaala ni jambo jema kwao kuweza kupata uelewa kwa wajumbe na menejimenti nzima ya VETA na kuwa itawazesha kujipanga katika utoaji elimu kwenye eneo lao la Elimu ya Amali.
Amesema, “Matarajio kwa wananchi ni makubwa kwenye maboresho ya mitaala hii hivyo ni wazi kuwa sasa kazi itaanza vyema ya kuhakikisha elimu imeboreshwa na kwamba sasa tunapaswa kujipanga vyema kama VETA.”
Katika hatua nyingine ,Dkt. Komba aliweza kukabidhi taarifa mbalimbali zilizofanyiwa kazi kwa VETA kupitia nakala laini (soft copy) zitakazosaidia katika utekelezaji wa rasimu ya mitaala.
Aidha, wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya VETA, wameipongeza sana WyEST na TET kwa kazi kubwa ya maboresho ya Mitaala na kuahidi kusimamia utekelezaji na kutekeleza kwa umahiri katika eneo lao la Amali.
Lengo na wasilisho hilo lililofannyika hii leo Oktoba 13, 2023 ni kuwapatia ufahamu Bodi na Menejimenti ya VETA kuhusu utekelezaji wa elimu ya Amali kwa Sekondari Hatua ya Chini ambapo utekelezaji wake kwa kiasi kikubwa utafanywa na kusimamiwa na VETA.