Mapigano yanaendelea katika jimbo la kusini mashariki mwa Sudan la Blue Nile kati ya makabila ya Hausa na Birta.
Walioshuhudia walisema maelfu ya waandamanaji wa kabila la Hausa waliweka vizuizi na kushambulia majengo ya serikali katika miji kadhaa Jumatatu, Julai 18.
Kulingana na maafisa wa afya, ghasia hizi zilizuka wiki moja iliyopita na zaidi ya watu 60 tayari wamekufa huku zaidi ya 150 wakijeruhiwa.
Mamlaka za usalama nchini humo tayari imepeleka jeshi katika eneo hilo, na kuweka amri ya kutotoka nje usiku sambamba na kupiga marufuku mikusanyiko katika baadhi ya miji.
Vyanzo vya ndani vinasema mapigano hayo yamechochewa na migogoro ya umiliki wa ardhi, huku wakiilaumu serikali ya kijeshi ambayo ilichukua madaraka kwa nguvu Oktoba mwaka jana kwa kuunda ombwe linalopendelea ghasia za kikabila.