Naibu Rais wa Kenya anayemaliza muda wake, William Ruto amesema ana uhakika wa kushinda uchaguzi huo na anaamini kuwa taifa hilo la Afrika Mashariki ni taifa la kidemokrasia na kwamba uchaguzi huo hautaingiliwa.

Ruto ameyasema hayo wakati wa kampeni zake zinazoendelea nchini humo, ikiwa zimebaki siku ishirini pekee kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

“Najua kuna dhana kwamba ukimuweka Rais wa sasa na kiongozi wa sasa wa upinzani upande mmoja inakuwa haiwezi kupingwa na ukweli ni kwamba watu wa Kenya wanaweza kukata na bado wakafanya uamuzi sahihi na nina imani kubwa kwamba nitashinda uchaguzi huu,” Ruto alisema.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta (katikati), akiwa na Naibu wake wa Urais William Ruto (kushoto) na Mwanasiasa Mkongwe Raila Odinga (kulia).

Katika uchaguzi wa urais uliopita wa mwaka wa 2017, rufaa ya Odinga ambaye aliamini kuwa ushindi wake uliibiwa huku kukiwa na mvutano mkubwa, ilisababisha uchaguzi huo kubatilishwa na Mahakama ya Juu ukiwa ni wa kwanza barani Afrika kupangwa upya.

Amesema, “Changamoto huwa zinakuja pale watu wanaanza kupiga simulizi, uchaguzi ukaibiwa, blablabla, huyu huyu huyu, na bahati mbaya sana kwa mshindani wangu safari hii hana wa kumlaumu kwa sababu serikali na kila kitu kiko upande wangu na ninadhani uchaguzi huu utakuwa wa amani.”

Kuhusu swali la wanahabari kuwa atafanyaje iwapo atashindwa, Ruto, ambaye aliwahi kushtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu kwa kuhusika kwake katika ghasia za 2007-2008, amesema kuwa uchaguzi huo utakuwa wa amani.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta (kulia), akiwa na Naibu wake wa Urais William Ruto (kushoto)

“Na ukiangalia ushindani uliopo, unahusisha watu kutoka makabila tofauti kila upande kwa hivyo tumeweza kwa kiasi kikubwa kujiondoa kwenye ushindani wa kawaida wa makabila na mambo ya aina hiyo hadi mahali salama wa kuweka umoja baina yetu,” amefafanua Ruto.

Chaguzi za kisiasa nchini Kenya, kwa mara kadhaa zimekumbwa na ghasia, hasa za kikabila, kama ilivyowahi kutokea mwaka 2007-2008 ambapo zaidi ya watu 1,100 walikufa, mamia kujeruhiwa na maelfu kuyakimbia makazi yao.

Rais Uhuru Kenyatta (kushoto) akiwa na kinara wa Upinzani Raila Odinga (kulia)

Young Africans kuweka kambi Dar es salaam
Odinga 'ajifagilia' asema yeye ni mradi