Serikali imeombwa kuongeza somo la utunzaji wa mazingira kuanzia elimu ya awali mpaka Chuo Kikuu ili kujenga utayari wa vizazi hadi vizazi kutunza mazingira.
Akizungumza na Dar24Media kupitia kipindi cha mahojiano, Katibu Mtendaji wa taasisi ta TanzaGreen Initiative (TAGRIN), Usman Mchinja amesema kuwa iwapo kutakuwa na somo la mazingira katika mtaala wa elimu, itasaidia kumjengea kila mtu hali ya utayari katika na nidhamu ya utunzaji mazingira.
“Ikiingia kwenye mtaala wetu kukawa na klabu za mazingira katika kila shule kila level kuanzia nursery(awali), primary school(shule ya msingi), Secondary School, Advanced school (sekondari), mpaka kwenye kila taasisi na kupitia hizi klabu kila mmoja atakuwa balozi wa mazingira,” amesema Mchinja.
Mchinja amesema kuwa kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kumjengea mtu tabia ya utayari katika kutunza mazingira, ambapo kwa miaka kumi ijayo Tanzania itaweza kuwa nchi yenye mazingira yaliyo salama.
Aidha, amesema kuwa elimu katika jamii ni muhimu sana kwani vita ya mazingira sio ya mtu mmoja, inahitajika serikali, taasisi hizo binafsi na jamii kwa ujumla kujiunga pamoja na kupambana na vita ya mazingira nchini Tanzania.
Mchinja amempongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo kwa kufungua kongamano la hifadhi ya mazingira na maendeleo endelevu na kuteua mabalozi wa mazingira na kusemakuwa uteuzi huo utakuwa msaada mkubwa katika kuboresha mazingira.