Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amesema Serikali imeyapokea maoni ya Wananchi kuhusu udhaifu wa vyombo vya uokoaji,. na kwamba inaenda kuyafanyia kazi na kujipanga ili kukabiliana na maafa kwa ufanisi pindi yanapotokea.
Bashungwa ameyasema hayo hii leo Novemba 7, 2022 wakati wa ibada maalum ya kuwaombea marehemu 19 waliofariki katika ajali ya Ndege mali ya Precision Air iliyotokea jana Novemba 6, 2022 wakati ikijiandaa kutua mjini Bukoba.
Kauli ya Bashungwa inakuja kufuatia watu wengi kulalamikia jinsi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilivyochelewa na kukosa vifaa sahihi kwa ajili ya kuwaokoa watu kwenye ajali hiyo iliyowagusa watu wengi nchini.
Katika ibada hiyo maalum ya kuwaaga marehemu, iliyofanyika hii leo Novemba 7, 2022 katika uwanja wa Kitaba ili kutoa heshima za mwisho kwa waliofariki, pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwaagiza Wakuu wa Mikoa husika kusimamia utekelezaji wa agizo la kugharamia mazishi.