Wito mpya wa pamoja, uliotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO, na lile la kazi duniani ILO umetaka kuchukuliwa kwa hatua madhubuti zinazohitajika za kukabiliana na changamoto za afya ya akili miongoni mwa wafanyakazi, kutokana na mwongozo mpya wa kimataifa kuhusu tatizo hilo na uwajibikaji kazini.
Ujumbe huo, uliowasilishwa kupitia chapisho unalenga ujumbe mmoja wa kushughulikia changamoto ya afya ya akili kazini ambayo ni na tamko la pamoja la kisera la WHO na ILO, yanakadiria kwamba takriban siku bilioni 12 za kazi hupotea kila mwaka kutokana na matatizo ya msongo wa mawazo na wasiwasi vinaougharimu uchumi wa dunia karibu dola trilioni 1.
Kwa mara ya kwanza, WHO inapendekeza mafunzo ya mameneja, ili kuwajengea uwezo wa kuzuia mazingira ya kazi yenye kuongeza shinikizo na kushughulikia ipasavyo na wafanyakazi walio katika changamoto.
Ripoti ya kimataifa ya WHO, kuhusu afya ya akili iliyochapishwa mwezi Juni 2022 ilionyesha kuwa watu bilioni 1 walikuwa wanaishi na matatizo ya afya ya akili mwaka 2019 , na asilimia 15 ya watu wazima wenye umri wa kufanya kazi walipitia matatizo ya afya ya akili.
Mwaka 2020, Serikali za ulimwenguni kote zilitumia wastani wa asilimia 2% tu ya bajeti zake za afya kwa ajili ya afya ya akili, huku nchi za kipato cha chini zikitenga chini ya 1% ya bajeti zake kwa ajili hiyo.