Marekani imetangaza kuwa itaanza tena kufadhili Shirika la Afya Duniani (WHO) na kujiunga katika ushirika unaolenga kugawanya chanjo ya virusi vya corona kote ulimwenguni huku Rais Joe Biden akitilia mkazo sheria za kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.
Hatua hiyo iliyotangazwa jana na Mshauri Mkuu wa Biden kuhusiana na janga la virusi vya corona, Dkt. Anthony Fauci, inafufua upya uungwaji mkono wa shirika ambalo uongozi wa Trump ulijitenga nalo.
Kujitolea haraka kwa Fauci kwa shirika hilo la WHO ambalo mikakati yake ya kushugulikia janga la virusi vya corona ilikosolewa na wengi, hasa na utawala wa Trump, kunaashiria mabadiliko katika hatua ya ushirikiano zaidi katika kukabiliana na janga hilo.
Fauci ameongeza kwamba anafurahia kutangaza kwamba Marekani itabaki kuwa mwanachama wa Shirika la Afya Duniani na kwamba Biden alitia saini barua zinazoondoa tangazo la awali la utawala wa Trump kujiondoa katika shirika hilo.
Hili ni tangazo la kwanza la umma la afisa wa serikali ya Biden kwa hadhira ya kimataifa na ishara ya kipaumbele ambacho rais huyo mpya ametoa katika vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 nchini humo pamoja na washirika wa kimataifa.
Wakati akitia saini maagizo 10 ya rais katika ikulu ya White House mara baada ya kula kiapo, Biden aliliambia taifa hilo kwamba idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 huenda ikaongezeka hadi nusu milioni kufikia mwezi ujao na kwamba hatua za dharura zinahitajika.