Marekani imedai kuwa vikosi vya China vinafanya mazoezi yenye nia ya kujiandaa kuishambulia Marekani na washirika wake katika Bahari ya Pacific.
Kwa mujibu wa ripoti ya makao makuu ya kijeshi ya Pentagon yaliyoko Washington D.C kwa Bunge la nchi hiyo, China imeongeza uwezo wake wa kutuma ndege za makombora umbali mrefu zaidi.
Imeeleza kuwa China imeendelea kuongeza bajeti yake ya kijeshi hadi $190 bilioni, ikiwa inaanza kuisogelea ile ya Marekani, kwa theluthi.
“Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, jeshi la China limeongeza kikosi chake na makombora kupitia njia ya maji, imepata uzoefu zaidi katika mapambano ya eneo la ukanda wa maji na huenda kufanya mazoezi kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya Marekani na washirika wake,” imeeleza ripoti hiyo.
Imefafanua kuwa kutokana na maandalizi pia ya makombora ya kutumia ndege za kivita, ni dhahiri kuwa China inaongeza uwezo wake wa kushambulia hadi eneo la Guam na ngome za kijeshi za Marekani za Magharibi mwa Bahari ya Pacific.
Ripoti hiyo pia imedai kuwa China inafanya maandalizi ya kutaka kuiunganisha kijeshi Taiwani na taifa hilo ili kujiongezea nguvu. Imeeleza kuwa inachotaka kufanya ni kuchelewesha uwezekeano wa Marekani kuingilia mpango wake wa kuiunganisha Taiwani.
Hata hivyo, China haijasema lolote kuhusu madai ya Marekani.
Nchi hizo mbili zimekuwa katika mgogoro wa kibiashara katika kipindi cha hivi karibuni.