Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema kuwa nchi yake haitaki vita na Iran, lakini ameapa wataendelea kuishinikiza Iran.
Ameyasema hayo wakati akijaribu kutuliza hofu ya jumuia ya kimataifa kuhusu kuongezeka mvutano unaohofiwa unaweza kuzidisha mzozo kati ya Marekani na Iran.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi habari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov katika mji wa Sochi nchini Urusi, Pompeo amesema kuwa Marekani haitafuti vita na Iran na kwamba Marekani imeweka bayana kwamba iwapo Iran itatishia maslahi ya nchi hiyo, basi kitisho hicho bila shaka kitajibiwa kwa njia inayoeleweka.
”Tunaitaka Iran ifanye mambo yake kama nchi ya kawaida, hilo ndilo tunaloliomba, tumeweka shinikizo katika uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kulifanikisha hilo. Kimsingi hatutafuti vita na Iran,” amesema Pompeo.
Aidha, matamshi yake yametolewa mara baada ya Marekani kupeleka Manowari ya kubeba ndege za kivita pamoja na ndege za mashambulizi aina ya B-52 katika eneo la Mashariki ya Kati, ingawa Rais Donald Trump amekanusha taarifa kwamba anafikiria kuwapeleka wanajeshi 120,000.
Wakati huo huo, kiongozi wa juu wa Kidini nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei amesema kuwa hakuna vita vyovyote na Iran wala mazungumzo mapya na Marekani na kwamba suala hilo haliwezi kutokea.