Ubalozi wa Marekani nchini, umesema kwamba haumuungi mkono mgombea yeyote au chama chochote katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 28 mwaka huu.
Kupitia taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya ubalozi wa Marekani Tanzania, ubalozi huo umesema kwamba licha ya kutokuwa na mgombea nchini, bado utafuatilia kwa karibu matendo ya watu wanaoingilia na kuvuruga mchakato wa kidemokrasia au kuchochea vurugu dhidi ya raia.
”Tunaunga mkono mchakato wa kweli wa uchaguzi huru, wa haki na wenye uwazi, kabla, wakati na baada ya siku ya uchaguzi. Hii ni pamoja na usalama wa wagombea wote, kuheshimiwa kwa utawala wa kisheria na hali ya mamlaka na vyombo vilivyopewa wajibu wa kusimamia na kuendesha uchaguzi kutokupendelea kabisa upande wowote,” umesema ubalozi huo.
Aidha ubalozi huo umesema kwamba unaunga mkono wito uliotolewa na wagombea wakuu wa kuwepo kwa mchakato wa uchaguzi wa amani na wenye uwazi na kutoa wito kwa wagombea na wafuasi wao kulinda amani na kuepuka matamshi ya kichochezi.
Taarifa hiyopia iliongezea kwamba historia ya Tanzania kuendesha chaguzi za amani imeifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika bara la Afrika.
”Historia ya Tanzania ya kuendesha uchaguzi zinazohusisha vyama vingi inarudi nyuma hadi miaka 25 iliyopita na kuifanya nchi hii kuwa mfano wa Kuigwa katika bara hili’, ilihitimisha taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.