Serikali ya Marekani imemualika aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kushiriki kongamano litakaloambatana na ziara ya wiki tatu kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu vita dhidi ya ufisadi litakalofanyika jijini Washington nchini humo.
Kafulila ambaye ameondoka usiku wa kuamkia leo, amekuwa mingoni mwa washiriki 12 walioalikwa kutoka barani Afrika ambapo watajifunza pia kuhusu mfumo wa uwazi na uwajibikaji nchini Marekani, mifumo ya manunuzi serikalini, mikakati ya kukabiliana na rushwa serikalini, nafasi za jumuiya za kiraia katika vita dhidi ya ufisadi na mengine mengi.
Kafulila ameuweka wazi uteuzi huo jana ikiwa ni siku chache tangu Rais John Magufuli amsifu kwa kuibua sakata la uchotaji wa zaidi ya shilingi bilioni 300 kwenye akaunti maalum ya Tegeta Escrow.
Akizungumzia uteuzi huo, Kafulila amesema kuwa ingawa watu wengi wanadhani kuwa umetokana na kauli ya Rais John Magufuli, uteuzi huo aliupata kabla ya kauli hiyo na kwamba kauli ya Rais iliongeza baraka juu ya hatua aliyokuwa ameifikia.
- JPM, Museveni kuweka jiwe la msingi mradi wa bomba la mafuta
- JPM aipa tano TCU, “nataka tuwe na nchi nzuri”
“Uteuzi huu ulifanyika kabla ya Mheshimiwa Rais kuzungumza kuhusu mimi. Lakini hata kabla ya hapo, taasisi inayounganisha wanaharakati Tanzania, kupitia chombo chao cha Watetezi wa Watetezi wa Haki za Binadamu walinipa tuzo ya wapiga filimbi (whistle blowers) kwa mchango wangu kwenye vita dhidi ya ufisadi,” amesema Kafulila.
Mwanasiasa huyo machachari anatarajia kurejea nchini Agosti 20 mwaka huu.