Mshambuliaji kutoka nchini Italia na klabu ya Nice ya Ufaransa Super Mario Balotelli, anawaniwa na klabu ya Malaga ya Hispania.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu za Liverpool na AC Milan, amekua na msimu mzuri tangu alipoelekea Ufaransa, hali ambayo imeanza kuonyesha matunda ya soka lake.
Mwishoni mwa msimu huu Balotelli atakua na maamuzi ya kusaini ama kutosaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu ya Nice ambayo ilimsajili kwa mwaka mmoja akitokea Liverpool mwanzoni mwa msimu huu.
Wakala wa mshambuliaji huyo mwenye sifa ya utukutu, Mino Raiola, ameripotiwa kuwa katika mazungumzo ya kina na viongozi wa klabu ya Nice pamoja na Malaga, na huenda akatangaza mustakabali wa mchezaji wake kabla ya msimu huu kumalizika.
Tayari Raiola ameshazungumza na viongozi wa klabu ya Malaga mara kadhaa, na taarifa zinaeleza kuwa, kuna dalili za uhamisho wa Balotelli mwishoni mwa msimu huu.
Hata hivyo hii si mara ya kwanza kwa wakala huyo kufanya hivyo, kwani aliwahi kuwa na mazungumzo na viongozi wa Malaga mwanzoni mwa msimu huu, wakati Balotelli akisaka mahala pa kujistiri, baada ya Liverpool kumuhakikishia hana nafasi ya kucheza, lakini siku chache baadae mshambuliaji huyo alijiunga na Nice ya Ufaransa.