Uongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Kigoma umetoa onyo kwa wadau wa soka mkoani humo, kuacha kasumba ya kulazimisha kuingia Uwanja wa Lake Tanganyika utakaotumika kwenye mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Julai 25, kati ya Mabingwa watetezi Simba SC dhidi ya Young Africans.
Katibu wa Chama Cha Soka Kigoma Omar Gimbi ametoa onyo hilo, baada ya kuchoshwa na tabia za wadau wanaaminika kuwa Wanachama na Mashabiki wa klabu hizo nguli kushinikiza kuingia uwanjani nyakati za usiku.
Gimbi amesema shinikizo kubwa la watu hao kutaka kuingia ndani ya Uwanja wa Lake Tanganyika ni kutaka kuchukua mchanga ili wakafanyie shughuli zao za kishirikina.
Hata hivyo kiongozi huyo amesema tayari ulinzi umeimarishwa Uwanjani hapo ili kudhihiti vitendo visivyokua vya kiungwana, ambavyo vinaweza kuleta picha mbaya kabla ya tarehe ya mchezo.
“Niwaonye mashabiki wa Simba na Young Africans watuache tumalize taratibu zetu, mambo ya kuja uwanjani usiku kuleta vitu vya hovyo, hivyo vitu vimepitwa na wakati.”
“Wanataka kuchukua mchanga ndio maana tumeweka ulinzi wa kutosha uwanjani”
Uwanja wa Lake Tanganyika kwa sasa upo kwenye maboresho ya mwisho kuelekea mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa Soka nchini na nchi jirani za Burundi, Rwanda na DR Congo ambazo zipo karibu na mji wa Kigoma.