Baada ya Kampuni ya Azam Media kusaini mkataba na klabu ya Young Africans juzi Alhamis (Julai 08) wenye thamani zaidi ya Shilingi Bilioni 30, Mkuu wa idara ya habari ya Ruvu Shooting Masau Bwire ameibuka na ombi lake.
Masau anaesifika kwa kauli za mvuto na zenye kufurahisha ameutaka Uongozi wa Azam Media kuifikiria na Ruvu Shooting katika uwekezaji mkubwa wa fedha kama ulivyofanya kwa Young Africans.
Masau amewasilisha ombi hilo kupitia andiko lake alilolichapisha kwenye kurasa zake za Mitandao ya Kijamii leo Jumamosi (Julai 10).
Masau ameandika: “Awali niipongeze sana? Young Africans kwa udhamini mnono walioupata kutoka Azam Media, ni udhamini ambao nina imani na hakika, ukitumiwa ilivyokusudiwa, utaiweka Klabu hii katika hatua nyingine ya mafanikio ya Kisoka, Tanzania, Afrika na Dunia.
Pia nimshukuru sana GSM ambaye jitihada zake katika kuijenga Young Africans kiuwezo na kiuchumi zinaonekana, nimemfuatilia na kumchunguza, nikabaini ni mtu sahihi na mwema kwa mafanikio na maendeleo ya Young Africans.
Si mchoyo, mng’ang’anizi wala mbinafsi, anahitaji ushirikiano na wengine, akiamini, nguvu ya umoja. Niwapongeze sana Azam Media kwa mahela haya wanayoyamwaga kwa ajili ya kuendeleza mpira wa Tanzania, Azam Media kwa sasa ni jiwe la pembeni kwa kulipa hadhi na heshima kubwa soka la nchi yetu.
Mungu azidi kuiimarisha taasisi hii! Ila, niwakumbushe tu kwamba, Azam Media, mnapochungulia juu huko, ebu jicho lenu pia litupieni huku chini, tupo kina Ruvu Shooting Star, mkifanya kitu huku, tutazidisha uimara wa ligi, na kuifanya iwe ya kuvutia, ushindani, mvuto na msisimko wa hali ya juu! Au, wadau wenzangu nyie mnasemaje?”