Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amezindua Mradi wa Kusambaza Umeme awamu ya pili katika maeneo ya pembezoni mwa jiji la Mwanza (Peri Urban).

Akizungumza na wananchi wa mtaa wa Igongwe, Kata ya Chibula Wilaya ya Ilemela, amesema kuwa Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 9 kuhakikisha kuwa inakwenda kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya umeme katika maeneo ya pembezoni mwa jiji hilo.

Amesema kuwa maeneo hayo wamechelewa kupata umeme kwakuwa hayakuwa na sifa ya kupata umeme wa 27,000 lakini kwasababu Serikali ni sikivu imeamua maeneo yote ya mjini yanayofanana na kijijini yapelekewe umeme kwa 27,000.

“ Tulipoanza kusambaza umeme vijijini tukajikuta tumepeleka umeme mwingi vijijini maeneo mengi ya mijini tena yana sura sawa na vijijini hayakuwa na umeme lakini kwasasa kutokana na mradi huu maeneo yote kama haya yatapata umeme wa bei nafuu,” Amesema Waziri Kalemani.

Aidha Waziri Kalemani, amemtaka mkandarasi kuhakikisha anasambaza umeme katika maeneo yote ya mitaa hiyo ndani ya miezi 12 ili wananchi wa maeneo hayo waanze mara moja kupata huduma hiyo muhimu huku akimsisitiza kutumia nguzo za zege ambazo zinadumu kwa muda mrefu.

Halikadhali amehasa taasisi kupewa kipaombele na wanachi kuhakikisha wanamaliza malipo ya kupata huduma za umeme ndani ya siku 14.

Nae, Meneja Miradi ya Umeme Vijiji, Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale, amesema mradi huo mkubwa unatarajia  kuunganisha umeme wananchi zaidi ya 10224.

Masau Bwire aiomba Azam Media kuwekeza Ruvu Shooting
Serikali imetenga Bilioni 1 ujenzi Taasisi ya Sayansi ya Bahari