Ushindi wa 2-1 dhidi ya Coastal Union umempa kiburi Afisa Habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire, kuelekea mchezo dhidi ya Young Africans utakaopigwa Jumatatu (Oktoba 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Jana Alhamis (Septemba 29) Ruvu Shooting ikicheza nyumbani Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, ilipata ushindi wake watatu msimu huu, mabao yakifungwa na Kiungo Mshambuliaji Rashind Juma.
Masau ametamba kuwa, kikosi chao kitakua cha kwanza kuifunga Young Africans ambayo imecheza michezo 40 ya Ligi Kuu bila kupoteza tangu msimu uliopita.
Masau amesema anaamini baada ya mchezo wa Jumatatu Ruvu Shooting itakuwa kileleni, kwani wana uhakika wa kushinda mchezo huo, licha ya baadhi ya mashabiki kuwabeza.
“Jumatatu baada ya mchezo wetu na Young Africans, tutakuwa tunaongoza Ligi. Msimu huu tumedhamiria Kuwa Mabingwa na tunataka kuwa sehemu ya historia ya nchi hii kwenye mabadiliko ya Mpira.”
“Kabla ya kutetema watakuwa wanatetemeka sababu wanajua wanaenda kucheza na Ruvu Shooting. Lengo msimu huu letu ni kufanya makubwa ndani na nje ya nchi.” amesema Masau Bwire
Ushindi dhidi ya Coastal Union, umeiwezesha Ruvu Shooting kufikisha alama 09, zinazoiweka nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.