Afisa Habari wa klabu ya Ruvu Shooting Masau Bwire amekubali kikosi chao kupoteza mbele ya mabingwa watetezi Simba SC.
Ruvu Shooting walikuwa wenye wa Simba SC katika mchezo huo uliochezwa leo Alkhamis (Juni 03), Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo uliokwishwa kwa wenyeji kukubali kufungwa 3-0, Masau amesema hana budi kukubaliana na matokeo hayo.
Amesema mchezo wa leo Simba SC walionesha kiwango kikubwa, tofauti na ilivyokua kwa upande wa kikosi chao, hali iliyopelekea kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao.
“Yote kwa yote uelewe tuseme tu hivyo, utaelewa tu taratibu lakini kwa ujumla mechi ya leo ni mzigo, ulikuwa mkubwa, meli imeelemewa, imezama.” Amesema Masau Bwire
Simba SC walipata bao la kuongoza kupitia kwa nahodha na mshambuliaji wao John Bocco dakika ya 17, kipindi cha kwanza.
Mshambuliaji kutoka DR Congo Criss Mugalu aliipatia Simba SC bao la pili dakika ya 62, huku Bocco akifunga bao la tatu dakika ya 86 kipindi cha pili.
Kwa sasa Simba SC imefikisha alama 67 , ikicheza michezo 27, ikifuatiwa na Young Africans yenye alama 61 zilizopatikana kwenye michezo 29.
Azam FC inashika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 60.
Wakati huo huo John Bocco amefikisha mabao 13 msimu huu kwenye ligi kuu na goli la 7 kwenye michezo 4 ya mwusho aliocheza.