Serikali imesema kuwa katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu nchi imeendelea kuwa katika amani na utulivu huku uhalifu ukipungua kwa asilimia 2.2 kwa makosa makubwa ya jinai ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita hali inayopelekea wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi kwa amani na usalama.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati akisoma taarifa ya Serikali mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, iliyohusu Hali ya Ulinzi na Usalama wa Raia na Mali zao kwa Kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka huu.
“Kuanzia Januari hadi Juni ndani ya mwaka huu jumla ya makosa makubwa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi nchi nzima yalikuwa 28,252 tofauti na kipindi kama hiki mwaka uliopita ambapo makosa 28,889 yaliripotiwa vituoni, tukiangalia vizuri hesabu zetu ndani ya mwaka huu tumepunguza makosa 637 hii yote inatokana na juhudi za askari wetu na utekelezaji wa dhana ya ulinzi shirikishi” amesema Mhandisi Masauni
Naibu Waziri Masauni ameyataja makosa hayo makubwa ya jinai kuwa ni Makosa dhidi ya binadamu, Makosa dhidi ya Maadili ya Jamii, Makosa ya kuwania mali na Makosa ya Uhalifu wa Kifedha.
Aidha, akizungumzia makosa ya usalama barabarani, Masauni amesema kuwa kumekuwepo na mafanikio katika kupunguza makosa ya usalama barabarani hali inayochagizwa na usimamiaji wa sheria na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu.
“Takwimu za makosa ya ajali za barabarani katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu zinaonyesha kuwepo kwa jumla ya makosa 1,610 yaliyoripotiwa ikilinganishwa na makosa 2,200 mwaka uliopita huku takwimu zikiweka wazi makosa 590 kupungua katika vipindi hivyo viwili” alisema Masauni
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema kuwa mafanikio hayo ya kupungua kwa uhalifu nchini yamechangiwa pia na matumizi ya teknolojia katika kupambana na uhalifu huku akiwaonya wahalifu kutafuta shughuli nyingine ya kufanya.
“Tunatumia vifaa maalum ikiwepo drones katika kudhibiti uhalifu japo kwasababu za kiintelijensia hatuwezi kusema ziko ngapi na maeneo gani muhimu tunawaasa wahalifu kuacha mipango yao ya kuvuruga amani ya nchi hii nawahakikishia hawatabaki salama, tunataka wananchi wafanye shughuli zao za kiuchumi,” amesema IGP Sirro
Vikao vya Kamati za Bunge vinaendelea jijini Dodoma huku wizara mbalimbali zikiwasilisha taarifa zao kwa kamati hizo huku vikao vya Bunge vikitarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi ujao.