Mbunge wa zamani wa jimbo la Nyamagana, Lawrence Masha ambaye aliwahi pia kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, amesema anaombwa kurejea kwenye nafasi ya ubunge wa jimbo hilo ambayo hivi sasa inashikiliwa na Stanslaus Mabula.
Masha ambaye amekuwa kimya kwa muda kwenye ulingo wa siasa, amesema wananchi wa jimbo la Nyamagana humtafuta wakimuomba agombee tena nafasi hiyo.
Akizungumza kwenye ‘The Joint’ ya Dizzim TV, Masha alisema kuwa moja kati ya mambo yalikuwa yanamshangaza ni kuzushiwa kuwa hakuwa karibu na wananchi na kwamba anaringa.
“Fitina na uongo viliwekwa kiasi kwamba zikakaa juu kwenye picha za watu, kiasi kwamba unajiuliza kweli mimi ndiye huyu wanayemuongelea… yaani ndio mimi huyohuyo!” Alisema Masha.
“Leo hii ninaulizwa, Masha tunakuomba urudi Nyamagana… mimi nilifanya kazi yangu vizuri. Wakati mwingine katika maisha kuna vitu watu watakuwa wanakusema hadi ukiyasikia unajiuliza kama ni wewe au la. Lakini sisi wanasiasa tunachokifanya huwa tunaweka ngozi ya mamba, unasemwa unaendelea,” aliongeza.
Alipoulizwa kama ana mpango wa kurejea kuwatumikia wananchi, alisema yuko tayari wakati wowote.
“Kama nitahitajika, niko tayari kwenda kuwatumikia wananchi, lakini sifanyi kwa ajili ya faida yangu,” alisema Masha.
Mwanasiasa huyo alikuwa Mbunge wa Nyamagana kwa mitano kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kisha akashindwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 na Ezekiah Wenje kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Katika joto la uchaguzi wa mwaka 2015, Masha alitangaza kuhamia Chadema. Lakini baada ya uchaguzi, mwanasiasa huyo alirejea CCM.