Wachezaji wawili wa klabu ya Benfica wamepata majeraha na kukimbiziwa Hospitali baada ya basi la timu hiyo kushambuliwa kwa mawe na mashabiki wenye hasira kali zilizosababishwa na matokeo ya sare tasa ambayo timu hiyo ilipata dhidi ya Tondela katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ureno.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imesema kwamba nyota hao waliokutana na dhuruba hiyo ni kiungo Mjerumani, Julian Weigl na winga Mserbia Andrija Zivkovic ambao walilazimika kukimbiziwa Hospitalini Jijini Lisbon ili kupata matibabu kwa haraka.
Tukio hilo lilijiri muda mfupi baada ya mchezo huo ambao ni wa kwanza kwa Benfica tangu Ligi Kuu ya Ureno isimamishwe mwezi Machi kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Licha ya kutokuwepo kwa mashabiki kwenye uwanja wa Da Luz ambao unatumiwa na Benfica kwa michezo yake ya nyumbani, gari hiyo ilishambuliwa na kikundi cha mashabiki ambacho kilikuwa nje ya uwanja huo, mara baada ya mchezo kumalizika.
Mashabiki hao walionekana kukasirishwa na matokeo hayo ambayo yamewanya kuwa na idadi sawa na wapinzani wao katika mbio za ubingwa, FC Porto kila timu ikiwa na alama 60 huku zikiwa zimebaki raundi tisa kabla ya ligi hiyo msimu huu kumalizika.
Uongozi Benfica umelaani kitendo hicho na kuahidi kushirikiana na mamlaka za ulinzi na za kisheria nchini humo kuwachukulia hatua wote walioshiriki vitendo hivyo.