Uongozi wa Simba SC umewataka Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kupuuzia taarifa zisizo sahihi za usajili unaohusisha klabu hiyo katika kipindi hiki ambacho wanakiboresha kikosi chao.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally amesema, katika kipindi hiki kutakuwa na maneno mengi ya uongo ya klabu hiyo kuhusishwa na wachezaji ambao hawapo kabisa katika malengo ya timu hiyo.

Amesema Simba SC wanaendesha mchakato wao wa usajili kwa siri kubwa na wanatoa taarifa pale kila kitu kinapokuwa kimekamilika.

“Wanachama na Mashabiki wetu wasifuatishe maneno ya mtaani, Simba SC ni Klabu kubwa na kwenye suala la usajili linaendeshwa kwa umakini na kila mchezaji tunayemtaka tutampata na kumtangaza pale kila kitu kitakapokamilika,” amesema Ally

Amesema katika kipindi hiki Simba SC inahusishwa na wachezaji wengi hata wale ambao hawapo kwenye malengo ya timu yao.

“Ukiangalia kwenye mitandao na vyanzo vingine, tetesi zimekuwa zikija kimkakati, lengo ni kuwavuruga Wanachama na Mashabiki wa Simba SC, ukiangalia kuna wachezaji ambao hawana sifa ya kuichezea Simba SC lakini wapinzani wetu wanawahusisha na sisi (Simba), lengo ni kuwavuruga Mashabiki na Wanachama wetu, niwaombe msifuatilie taarifa za kwenye mtandao, taarifa sahihi zitatolewa na klabu kwenye ‘Platfomu’ zetu,” amesema Ally.

Amesema kinapokuja kipindi cha usajili kuna mikakati mingi ikiwa pamoja na kuwatangaza wachezaji ambapo mameneja wa wachezaji hao wanatumia klabu kubwa kama Simba SC kuwatangaza wachezaji wao hata kama Simba SC haina mpango nao.

“Yaani mchezaji Simba SC hatuna mpango naye, lakini unasikia tunamtaka, viongozi wamezungumza naye, au wamemsafirisha, halafu inakuja kuibuka taarifa kuwa mchezaji amechukuliwa na klabu nyingine na hii inafanywa makusudi ili mashabiki waone wamepokonywa mchezaji na lawama zielekezwe kwa viongozi wetu, mashabiki wetu watulie taarifa kamili kwa kila mchezaji tunayemtaka na kumsajili watazipata kupitia kwa viongozi na Platfomu zetu,” amesema Ally.

Uongozi wa Simba SC kwa sasa upo kwenye mchakato wa kuimarisha kikosi chao huku wakiweka wazi kufanya usajili kutokana na matakwa ya Kocha wao Robert Oliviera ‘Robertino’.

Mgawanyo jimbo la Mbeya: Dtk. Tulia amtaja Magufuli
Slaa aunga mkono uwekezaji, aishauri Serikali mkataba wa DP World