Serikali ya Syria imeanzisha mashambulizi ya ardhini katika eneo linalodhibitiwa na waasi Ghouta Mashariki licha ya mpango wa Urusi wa kusitisha mapigano kwa muda wa saa tano kila siku.
Shirika la haki za binaadamu lenye makao yake nchini Uingereza limesema kuwa mashambulizi ya mabomu yalifanyika jana mchana Ghouta Mashariki, huku kukiwa hakuna dalili ya kupelekwa misaada katika eneo hilo ambalo limezingirwa.
Aidha, Shambulizi la jana lililenga eneo la Hawsh al-Dawahra lililoko ukingoni mwa Ghouta Mashariki ambapo waasi wameweka ngome yao.
Urusi imesisitiza mpango wa kusitisha mapigano kwa muda wa saa tano kila siku ili kuwezesha misaada ya kibinaadamu kupelekwa katika eneo hilo na kuruhusu raia na majeruhi kuondolewa.
Hata hivyo, Marekani na Urusi zinatupiana lawama kwa kushindwa kuheshimu mkataba wa kusitisha mapigano Ghouta Mashariki, kwa siku 30 ambao ulipitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumamosi iliyopita.