Siku chache baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kufuta mashtaka 14 yakiwemo ya ugaidi yaliyokuwa yakiwakabili masheikh 36 wa Uamsho, aliyekuwa anawahudumia gerezani amesimulia yaliyowakuta.
Ilyasa Mohamed Bakari, ambaye alijitambulisha kama kiongozi wa watu waliokuwa wanawahudumia masheikh hao walipokuwa gerezani, kwa kuwapelekea chakula kwa kipindi chote cha miaka minane, amefanya mahojiano maalum na Gazeti Mwananchi na kueleza magumu waliyopitia.
Bakari amesema kuwa walichaguliwa watu watatu kuwahudumia masheikh hao, ambapo familia zilikuwa zikichangia huduma pamoja na vyakula wanavyopelekewa.
Mhudumu huyo amesimulia kuhusu vikwazo walivyokutana navyo mwaka 2017, baada ya kufika kwenye gereza la Segerea wakiwa na ndoo za vyakula na kisha wakaambiwa kuwa mahabusu hao wamehamishiwa katika Gereza la Ukonga.
Anasema walilazimika kurudi na vyakula hivyo na kuwapatia watoto yatima, kisha kuelekea Gereza la Ukonga ambako walikutana na masharti mapya na magumu kwao.
“Tulipofika Ukonga tuliambiwa lazima tupate vibali vipya maana vibali tulivyokuwa navyo vilikuwa ni kwa ajili ya Segerea tu, kwa hiyo zile ndoo mbili za chakula na nyingine ya mchuzi tulilazimika kurudi nazo na kuzipeleka kwa watoto yatima,” Bakari aliliambia Gazeti Mwananchi.
Aidha, alisema walifanikiwa kupata vibali hivyo, lakini wakakutana na sharti jipya la kupeleka chakula siku za Jumamosi na Jumapili pekee, badala ya utaratibu wa kila siku. Pia, walipewa sharti kuwa ni lazima kila mahabusu ahudumiwa na watu watatu, kwahiyo walipaswa kuongeza idadi ya wahudumu kuwa 108.
Anasema walijaribu kukidhi vigezo vya sharti hilo lakini kutokana na uchumi wa familia husika, walishindwa kutimiza idadi iliyokuwa inahitajika.
Sambamba na hilo, utaratibu wa kuingiza chakula chote kwa mahabusu ulibadilika, badala yake ikawa wanapopeleka chakula kinapimwa kwenye bakuli na kingine wanarudishiwa.
Mashekh hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya ugaidi wakidaiwa kufanya makossa hayo visiwani Zanzibar na Dar es Salaam, kati ya Januari 2013 na Juni 2014, kinyume cha Sheria ya Ugaidi ya Mwaka 2002.
Juni 14, 2021 waliachiwa huru na kuungana na familia zao. Kwa mujibu wa Bakari (kiongozi wa wahudumu wao), alisema masheikh hao wamepelekwa hospitali kufanyiwa vipimo ili kufahamu hali ya afya zao kwakuwa wamekaa gerezani kwa muda mrefu. “Tunataka waangalie afya zao kwanza kwa sababu ndio jambo la msingi baada ya kutoka gerezani. Baadhi yao walionekana kudhoofika afya, lakini wengine wapo imara,” Bakari anakaririwa