Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa amekagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa na maabara katika Shule ya Sekondari ya Hawa Mchopa iliyopo katika kata ya Malolo wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi.
Akizungumza na Walimu, wanafunzi na wananchi kwenye viwanja vya shule hiyo, Waziri Mkuu amesema kuwa shule hiyo inatarajia kupokea wanafunzi 126 wa kidato cha tano kwa mara ya kwanza katika muhula wa masomo unaoanza Julai 3, 2021.
Amesema hatua hiyo ni mpango wa serikali katika kuhakikisha kwamba inainua na kuboresha sekta ya elimu nchini.
Amesema kuwa hatua ya kuanza kutoa mafunzo ya elimu ya kidato cha tano na sita katika shule hiyo itasaidia kuibua hamasa kwa wanafunzi wengine wa vidato vya chini.
“Siri ya mafanikio kwenye elimu ni mashindano ya kitaaluma, hawa wa vidato vya chini watashawishika kusoma kwa bidii wakilenga kufaulu ili waingie kidato cha tano na baade kusoma elimu ya juu zaidi”amesema Majaliwa
Waziri Mkuu amesema kuwa serikali itaendelea kusimamia shughuli za maendeleo katika sekta zote ikiwa ni pamoja na elimu, huduma za maji safi na salama na usambazaji wa umeme katika maeneo yote nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amemuhakikishia Waziri Mkuu kuwa ataisimamia sekta ya elimu katika mkoa huo na kuhakikisha kwamba watoto wanapata elimu bora na walimu wanafundisha katika mazingira mazuri.
Aidha ametoa wito kwa wazazi kuwasomesha watoto wao kwa sababu kitendo hicho ni sawa kabisa na uwekezaji mkubwa utakaowafanya wazazi kuwa matajiri pindi watoto watakapomaliza masomo yao na kuanza kuwasaidia wazazi wao.